Pia ameitisha Bunge la 11 ambapo wabunge watakutana mjini Dodoma kuanzia Novemba 17 hadi 19 na atapeleka jina la Waziri Mkuu ambaye atamteua kwa ajili ya kuidhinishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Dk Magufuli amefanya uteuzi huo saa chache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania.
Alisema Dk Magufuli katika kuonesha utendaji wake wa kazi kwa kufuata sera ya hapa kazi tu amechukua uamuzi huo saa chache baada ya kuingia ofisini kwake.
Dk Magufuli aliwasili Ikulu ambapo baada ya kupokelewa na wafanyakazi alienda moja kwa moja ofisini kwake na kufanya uteuzi huo kabla ya kuungana na wageni wake kwa chakula cha mchana. Sefue alisema Mwanasheria Mkuu huyo anaapishwa leo katika Viwanja vya Ikulu saa nne asubuhi.
“Kwa kawaida kabla ya uteuzi mwingine ni lazima Rais ahakikishe kuwa anamteua Mwanasheria Mkuu kwanza na ndipo wengine wanafuata na hiyo ameianzia leo (jana),” alisema Balozi Sefue. Pia Balozi Sefue alisema kuwa Rais Dk Magufuli ameitisha Bunge, Novemba 17 na kuongeza kuwa siku mbili baadaye atapeleka jina la atakayemteua kuwa Waziri Mkuu.
“Kwa mujibu wa Katiba Rais anatakiwa ndani ya siku zisizopungua 14 ahakikishe kuwa anamtangaza Waziri Mkuu wake na kwa kuonesha umakini zaidi huyu amechukua muda mfupi zaidi kufanya hilo kwa kuwa si mnajua kuwa huyu ni mtu wa kazi tu,” alisema Balozi Sefue.
Pia Balozi Sefue aliongeza kuwa Rais Magufuli ameonesha mfano kwa marais wengi hasa wa Afrika kuwa siasa ni urafiki na sio uhasama hasa kwa kuwakaribisha wanasiasa wote hata wa upinzani katika dhifa iliyofanyika kuanzia kuapishwa, chakula cha mchana pamoja na cha usiku.
Alitoa hoja hiyo alipojibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata mtazamo wake kutokana na kitendo cha kushikana mikono pamoja kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata pamoja na mpinzani wake wa kisiasa, Raila Odinga ambao wawili hao walihudhuria sherehe za kuapishwa Dk Magufuli na kisha kukutana Ikulu.
EmoticonEmoticon