MKULIMA WA BANGI ANASWA HUKO SONGEA

Mkulima wa bangi anaswa

Mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi na pingu mkononi wakati askari aking’oa bangi hizo shambani.

KIBANO! Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limemnasa mkulima mmoja, Kiliani Fussi (pichani) kwa tuhuma za kulima bangi kwa kificho kwenye shamba lake maalum huku akijua ni kosa kisheria, twende na Risasi Jumamosi.

Polisi wakijadiliana jambo

Zoezi hilo lilifanyika hivi karibuni ambapo mkulima huyo alishtukizwa na askari akiwa kwenye shamba hilo lenye ukubwa wa nusu eka ambalo lipo kwenye Mtaa wa Namanyigu katikati ya Manispaa ya Mji wa Songea.

…wakiichoma moto bangi hiyo

Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa, Revacus Malimi walilifikia shamba hilo kwa tabu kwani njia ya kuelekea ilikuwa ina majani aina ya upupu ambayo yana sifa ya kuwasha hali iliyowalazimu polisi hao kuyafyeka kwanza majani hayo ili kuweza kupita kwa urahisi.

Polisi wakifanya ukaguzi shambani humo.


Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo kwa nyakati tofauti  waliliambia Risasi Jumamosi kwamba, Fussi amekuwa  mkulima wa siku nyingi wa mmea huo haramu lakini huwa analindwa na baadhi ya viongozi licha ya raia wema kutoa taarifa.

Walisema kuwa, majirani wenzake ambao wanalima katika eneo moja mazao ya chakula na biashara walijaribu kumuonya kuhusu ulimaji wa zao hilo, lakini hakuwasikiliza.

Kama kawaida yake, Risasi Jumamosi lilimdaka Kamanda Msikhela ili aweze kuzungumzia sakata hilo la ukomeshaji wa kilimo haramu cha bangi nchini ambacho kimekuwa kikileta madhara makubwa kwa jamii ambapo alisema:

Shamba la bangi

“Jeshi la polisi lilifanikiwa kukamata shamba hilo la bangi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema. Mtuhumiwa tumemkamata na taratibu za kisheria zinaendelea ili afikishwe mahakamani.”

Kamanda Msikhela aliwataka wananchi, kuendelea kutoa taarifa za siri kwa jeshi la polisi punde wanapobaini kuwepo kwa uvunjwaji wa sheria za nchi katika maeneo yao.

Source;Global



EmoticonEmoticon